Serikali
imetangaza kusimamisha kupokea wakimbizi kutoka nchi za Maziwa Makuu
kwa makundi, kutokana na kutokuwepo kwa sababu za kiusalama,
zinazowafanya wakimbizi hao kukimbia nchi zao na kuomba hifadhi ya
ukimbizi nchini.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametoa kauli hiyo ya
serikali mjini Kigoma wakati wa uteketezaji wa silaha haramu,
lililofanyika kikanda mkoani Kigoma, na kueleza kuwa kwa sasa hakuna
tena wakimbizi watakaoingia kwa makundi watakaoruhusiwa kuingia nchini.
Mwigulu
alisema serikali itawapokea wakimbizi mmoja mmoja na kila atakayeingia
atahojiwa na mamlaka zinazohusika na mamlaka zikijiridhisha kuwa
anastahili hadhi ya ukimbizi, atapokewa na kupelekwa kwenye kambi za
wakimbizi zilizopo, kwani hakuna tena kambi ya wakimbizi
itakayofunguliwa kwa sasa.
Alisema
serikali kwa kutumia vyombo vyake, imejiridhisha kwamba hakuna hali
mbaya ya usalama, inayowakimbiza raia hao kutoka kwenye nchi zao na
kwamba zaidi imegundulika kuwa wengi wao wanakimbia kwa sababu za
kiuchumi, kuja kutafuta namna ya kuishi ili kukidhi hali zao za maisha.
Alisema
uwepo na uingiaji wa wakimbizi nchini, umekuwa na mchango mkubwa katika
uzagaaji wa silaha haramu sanjari na kuongezeka kwa matukio ya utumiaji
wa silaha na kuathiri uchumi na maisha ya watu mbalimbali.
Katika
hatua nyingine, waziri huyo amesema serikali imefuta utaratibu wa kutoa
uraia kwa makundi, kama ilivyofanya kwa wakimbizi wa Burundi waliopo
nchini. Alisema kwamba kwa sasa uraia utatolewa kwa mtu kulingana na
maombi yake.
Alisema
ukarimu huo wa Watanzania, umekuwa na athari kubwa katika ulinzi na
usalama nchini, hasa mikoa ambayo imewahifadhi watu hao kutokana na
kuongezeka kwa vitendo vya mauaji, ujambazi wa kutumia bunduki, lakini
kupanda mbegu mbaya ya kuuana kwa kulipiza visasi ambavyo vimekuwa
vikifanywa na raia hao waliopewa uraia.
“Kwa
mamlaka niliyopewa, natoa amri ya kusimamisha kutoa uraia kwa makundi
kama ambavyo imetoa Tanzania na haijawahi kutokea nchi nyingine, tumeona
athari kubwa ya watu hao na sasa sehemu kubwa ya Mkoa wa Tabora imekuwa
na hali mbaya kiusalama na tabia ya kulipizana visasi,” alieleza Mwigulu.
Akitoa
taarifa kwa waziri, Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la
Polisi, Marijani Nsato alisema silaha haramu 5,608 zikiwemo bunduki za
kivita, zilitarajia kuteketezwa. Nsato alisema katika silaha hizo,
kulikuwa na bastola 21, Shortgun 606, SMG 166, Riffle 300, bastola
bandia 21, FN Riffle 3, G3 moja, SAR 3 na magobore 4487.
Sanjali
na bunduki hizo, aliitaja mikoa ambayo imeshiriki katika kuchangia
bunduki haramu zilizoteketezwa kuwa ni Kagera 100, Rukwa 189, Katavi 81,
Simiyu 16, Mwanza 88, Geita 82, Mara 80 na Kigoma ukiwa na jumla ya
bunduki 424 ambazo zimeteketezwa katika kazi ya jana.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga alisema mkoa huo
kuwa mpakani na kupokea idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi za Maziwa
Makuu, kumechangia mkoa huo kuathirika kwa kiasi kikubwa na uzagaaji
silaha haramu na matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha.
Alisema mkoa utaendelea kuweka mkakati wa kudhibiti silaha haramu na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.
0 comments:
Post a Comment